TEL: +255 752 920 592

UKWELI KUHUSU MALENGO YAKO

Mwanzo wa mwaka 2021, ulipanga malengo makubwa ukiwa na hamasa kubwa na matumaini kuwa mwaka 2021 ndio mwaka wako wa kubadili maisha yako kwa kutimiza malengo yako.

Miezi sita imepita, swali la kujiuliza je, umetimiza malengo yako kwa asilimia ngapi?

Baada ya vikwazo, changamoto pamoja na matatizo, umepoteza hamasa na kuona mwaka huu ni mgumu kwako kutimiza malengo yako na kuanza kuamini labda mwakani au miaka ijayo ndio utaweza kutimiza malengo yako.

Ngoja nikueleze muda unatosha kabisa kwako kutimiza malengo yako kwa muda uliopanga, Je una malengo yanayoeleweka na kuwa na sifa ya kuwa malengo ambayo yanapimika na kutimizika?

Hujachelewa kutimiza malengo yako maana kuna miezi mingine sita imebaki kabla ya mwaka kuisha wa 2021.

Hivyo, kabla ya kuendelea ,naomba ufahamu sifa ya malengo yanayoeleweka ili mwisho wa siku mwaka ukiisha uweze kutimiza malengo yako uliyopanga;-

1. Lazima lengo lako limeandikwa

Kugeuza matamanio pamoja na ndoto zako ambazo unazo, hakikisha unaandika sehemu ambayo utakuwa unapitia. Inaweza kuwa kwenye diary yako, notebook au daftari lako. Moja kwa moja ndio huitwa lengo na kuwa na sifa ya kuwa lengo linalo eleweka. Mfano, una ndoto ya kuwa mfanyabiashara na unatamani kuwa mfanyabiashara mkubwa, kitendo cha kuandika matamanio yako pamoja na ndoto yako, umegeuza kuwa lengo la kuwa mfanyabiashara.

2. Lazima uwe umeandaa mpango mathubuti

Mpango unaonyesha njia gani upite ili uweze kutimiza lengo lako, mikakati gani unayo ili uweze kutimiza lengo lako. Ili upate matokeo mazuri, ni lazima mpango wako uwe na uwiano na lengo lako, mfano; ili ufanikishe lengo lako la kuwa mfanyabiashara basi ni lazima uwe mpango mathubuti ambao ni mpango biashara (business plan).

3. Lazima kuwe na ukomo wa muda wa kutimiza lengo lako (deadline)

 Unategemea lengo lako utatimiza ndani ya muda gani? Unapoweka ukomo wa lengo lako, Unajenga nidhamu na kuongeza ufanisi wa kutimiza lengo lako, hivyo inaweza kuwa miezi mitano, miezi kumi, miaka miwili au miaka mitano.Hiiinategemea na ukubwa wa lengo lako, mfano lengo la kuwa mfanyabishara, unategemea utakamilisha ndani ya miezi sita ya kwanza.

4. Lazima lengo lako liwe na eneo/sehemu maalumu,

Sio kila eneo linafaa kutimiza malengo yako/lengo lako hivyo ni muhimu kujua eneo gani unapaswa kuwepo ili uweze kutimiza lengo lako, mfano lengo lako ni kuwa mfanyabiashara wa nguo na upo sehemu ambayo uhitaji wa nguo ni mdogo au hamna kabisa, haiitakuwa rahisi biashara yako ya nguo kufanikiwa, hivyo ni lazima kujua unataka kutimiza lengo lako sehemu gani.

Kupanga na kuwa malengo ni hatua ya kwanza, hatua ya pili na muhimu ni utekelezaji wa kuyafanikisha malengo yako, na hapa ndio tofauti ya wanao timiza malengo yao na wanaokuwa na malengo pasipo kuyatimiza.

Ili kutimiza malengo yako, hamasa pekee haitoshi kufanya utimize malengo yako. Je Ukiwa hujisikii kabisa kutimiza malengo yako na hamasa umepoteza huwa unaendelea kupambana kutimiza malengo yako au unasubiri hamasa irudi na ndio utimize malengo yako?

Hamasa haitoshi kabisa, hivyo ili uweze kutimiza malengo yako hakikisha una nidhamu  kubwa na halisi.  Tazama  Kanuni hii;

 Hamasa + Nidhamu= Kutimiza Malengo Yako.

Kupitia Kanuni hii, unaona nguvu ya nidhamu kwenye kutimiza malengo yako kwa sababu hata hamasa ikipungua unaendelea kupambana kutimiza malengo yako. Hii ni sababu nidhamu inakupa nguvu ya kuendelea pasipo kujali unajisikia au hujisikii utaendelea kutimiza malengo yako.

Hamasa jumlisha nidhamu utaweza kutimiza malengo yako, nidhamu ambazo unapaswa kuanzia kuzijenga ni pamoja na;-

1. Nidhamu ya kuwajibika

Hakuna mtu ambaye atakuja kwenye maisha yako kukutimizia malengo yako isipokuwa wewe mwenyewe! Amua kuchukua uwajibu wa asilimia mia moja (100%) juu ya maisha yako na malengo yako, hivyo acha kuwatupia lawama watu wengine mzigo wa kushindwa kutimiza malengo yako. Ni lazima uwajibike kikamilifu Zaidi, ili uweze kutimiza malengo toka siku unapanga, mpaka unakamilisha. Utafanikiwa kwa kuacha tabia ya uvivu, visingizo, kughairisha pamoja na lawama na kuanza kuwajibika kwenye kila hatua ya maisha yako na  malengo yako.

2. Nidhamu ya maarifa

Lazima kua na uthubutu kwa kujitoa kikamilifu kutimiza malengo yako kwa muda uliopanga. Fanya hivi kwa kujifunza kila siku, kwa kuongeza maarifa kupitia kusoma vitabu, kusikiliza audbooks, Podcast, kuhudhuria semina, kusoma makala kwenye mitandao ya kijamii pamoja kushiriki kwenye mijadala chanya Ili uongeze hekima.Mfano, ili utimize lengo lako kuwa mfanyabishara, lazima uwe na maarifa ya kutosha kuhusu biashara kupitia kujifunza kutoka vyanzo mbalimbali vya maarifa. Mtu mmoja mwenye hekima aliwahi kusema “Siku ambayo utaona unajua kila kitu kwenye maisha yako, ndio siku ambayo unakaribisha anguko kubwa kwenye maisha yako” jifunze kisha fanyia kazi uliyojifunza.

3. Nidhamu ya muda

Mwandishi mmoja aliwahi kusema “Muda unatosha kabisa kutimiza malengo yako, lakini hautoshi kabisa kufanya kila kitu kwenye maisha yako”. Muda wako unatumia kwenye mambo yanayo chochea kutimiza malengo au mambo yanayokuweka mbali na malengo yako? Rasimali muda ndio rasimali pekee ambayo haina mbadala, hivyo Ili utimize malengo yako ni lazima uongeze nidhamu ya muda kwenye kupangilia muda wako kuanzia ratiba ya siku, wiki na mwezi utafanya nini ili utimize malengo yako pia kuweka vipaumbele kwenye kufanikisha malengo yako. Kumbuka muda unatosha kabisa kama utautumia muda ipasavyo kwa kupunguza kufanya mambo ambayo sio ya umuhimu kwenye maisha yako, kama kufuatilia maisha ya watu wengine, kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mrefu, pamoja na kufuatilia habari ambazo hazikujengi kwa namna yeyote ile na kuanza kufanya mambo ya muhimu.

4. Nidhamu ya marafiki

 Warren Buffett mwekezaji maarufu marekani na mwenye hisa kubwa kwenye kampuni ya Coca cola aliwahi kusema “Nionyeshe marafiki zako watano ambao unashinda nao muda mwingi, na mimi nitakuambia wewe ni mtu wa aina gani”. Marafiki wana mchango mkubwa kwako kufanikisha kutimiza malengo yako au kutotimiza malengo yako, hivyo kuwa makini kwa kujiuliza je marafiki zangu ni chachu ya mimi kupambana zaidi kutimiza malengo yangu? Au ni chanzo cha mimi kuridhika na kukata tamaa juu ya malengo yangu? Jitahidi sana kuwa na marafiki wenye maono makubwa, wapambanaji, wanakuambia ukweli pale unapokosea, wana wajibika na wanaishi uhalisia wa maisha yao.

5. Nidhamu ya fedha

Mwandishi wa vitabu vya fedha Dr Amani Makirita aliwahi kusema “Kanuni rahisi ya kuelekea uhuru wa kifedha ni kuanza kujilipa kwanza wewe mwenyewe  kabla ya kuitumia fedha yako kwenye matumizi mengine”.  Je, fedha zako unazipangilia kwa maana kuweka bajeti? Unaishi chini ya kipato chako kwa maana matumizi ya fedha zako yapo chini ya kipato chako? Unatumia fedha zako kwenye kuyafanikisha malengo yako? Una utamaduni wa kwa kujilipa wewe mwenyewe kwanza na kuweka akiba? Nidhamu ya fedha ni pamoja kujua namna ya kuzalisha fedha, kusimama fedha na kutunza fedha.

Kumbuka kutimiza malengo yako sio jambo la siku moja lakini kutimiza malengo yako ni mchakato ambao unachukua muda kabla ya kupata mafanikio/matokeo yenyewe.

Ukweli kuhusu malengo yako ni kwamba kutimiza malengo yako unahitaji kuwa na nguvu ya nidhamu kubwa na halisi ndio msingi wa kutimiza malengo yako.

Tunakutakia utekelezaji mwema.

Muandishi wetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.