TEL: +255 752 920 592

Shujaa wa Mwezi

Naitwa Maureen Ian Rizdel

Mimi ni mwalimu kitaaluma na mjasiriamali kwa hiyari.

Niliamua kuiita kampuni yangu Instanbul2Dar kwa lengo la kuunganisha majiji makubwa kibiashara ya Instabul na Dar es Salaam yaani kutoka Ulaya kuja Afrika. Instabul ni jiji kubwa nchini Uturuki na Dar es Salaam ni kitovu cha biashara Tanzania na moja ya majiji yanayokua kwa kasi barani Afrika.

Istanbul2dar ni kampuni inayojishughulisha na upatikanaji wa bidhaa za rejareja na jumla kutoka Uturuki kuja Tanzania. Ili kuchagiza ukuaji wa biashara wa kila mtu, tunaangazia wafanyabiashara wote yaani wadogo na wakubwa.

Mbali na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara hao, Istanbul2dar kwa upande wa pili inatoa huduma kama duka la rejareja kwa kimombo ‘Retail store’.  Kwa wale wanaopenda mavazi yenye ubora na yanayoendana na fasheni, wanaweza kupata viwalo kuanzia vya watu wazima mpaka vya watoto kike na kiume.

Namna safari yangu ilivyoanza

Wakati nikiwa mwanafunzi wa chuo nilipata fursa ya kuja kusoma nje Shahada ya Elimu (Bachelor Degree in Education) jijini Instabul, Uturuki ili niwe mwalimu. Kipindi hicho nilikuwa naangalia na kujifunza masuala ya biashara nje ya masomo yangu.

Siku zote akili yangu huwa inapenda kujifunza zaidi namna ya kuongeza kipato changu. Siku moja nilikuwa kwenye eneo kubwa la maduka (mall) huku nikiangaza huku na huko na kuona ‘brands’ (nembo) kubwa za biashara za mavazi na fasheni kama H&M, ZARA, MANGO na maduka mengi ya nguo ya hapa Uturuki ambayo hayapo nyumbani Tanzania.

Haraka haraka nikapata wazo kuwa naweza kupata kipato kupitia biashara hii badala ya kuwa mnunuaji na mtumiaji mkubwa wa fedha kama wanafunzi wengi.

Nikawaza, hivi kama nina Dola za Marekani 100 kwa ajili ya kujikimu kwa nini nisianze kununua na kuuza bidhaa. Hizo ndizo fikra zilizochagiza kuanzishwa kwa biashara ndogo mtandaoni miaka sita iliyopita.

Wakati naanza biashara hii nilikumbana na changamoto nyingi ikiwemo kupata sapoti kidogo kwa vijana wenzangu. Nilikuwa nimezungukwa na vijana wanafunzi ambao nadhani kwa kipindi kile waliona biashara hii ya kuzunguka madukani na kuuza mtandaoni ilikuwa ni kama ni kupoteza muda tu. Pamoja na kupata sapoti ndogo, binafsi sikujali na niliongeza nguvu ili kujenga msingi wa leo.

Pamoja na yote hayo, changamoto kubwa ilikuwa ni nani ataisimamia biashara yangu kwa upande wa Tanzania kwa sababu mimi naishi Uturuki. Haikuwa rahisi ila nimepambana.

Ninajiamini na napenda sana kujaribu kufanya jambo bila kuhofia ‘risks’ (vitahatarishi). Nipo tayari kufanya jambo lolote ambalo ninaona lina fursa ya kutengeneza hela.

Usikubali kurudishwa nyuma

Kama unavyoona katika safari yangu motisha ilikuwa inatoka ndani mwangu na naamini hata wewe utachagua aina ya maisha unayotaka kuishi. Ukiamua kulala basi maisha nayo yatalala na ukiamua kuamka na kutafuta basi lazima mwisho wa siku utavuna tunda unalostahili.

Nilibaini tangu awali kuwa iwapo nataka mabadiliko hapana shaka natakiwa kuanza mwenyewe taratibu na hakuna mtu atakayenifanyia hayo mabadiliko.

Faida yangu ya kwanza ilikuwa Dola za Marekani 500 (Sh1,150,000) lakini wakati naanza biashara hii lengo langu halikuwa sana katika kutengeneza faida bali kutafuta chanzo kingine cha mapato hapo baadaye nje ya kazi yangu ya ualimu.

Nasema lengo kubwa halikuwa faida kwa wakati huo kwa kuwa kipindi hicho ilikuwa ni ndogo kiasi kuwa haiwezi kukufanya uifurahie ila niliamini siku zijazo ikichanganywa na mshahara wangu huenda ingenifikisha mahali katika kumudu gharama za maisha.

Jambo la msingi nalotaka kueleza hapa ni kuwa siku zote lengo langu ni kutotegemea chanzo kimoja tu cha mapato katika maisha yangu.

Siku ya kwanza au siku moja? Ni chaguo lako

Kiukweli nimeweza kukuza biashara hii Kwa sababu ya juhudi na nguvu nilizoweka siku za nyuma. Mafanikio makubwa au madogo hayaji ndani ya siku moja. Nilianza kwa kusafirisha boksi moja la kilo 30 kwa mwezi miaka ya nyuma lakini leo hii baada ya miaka kadhaa nimeweza kutuma boksi zaidi ya 50 kwa wiki. Hii ina maana kuwa biashara yangu imekua mara dufu. Ingekuwaje, ningekata tamaa?

Akiba ya fedha ni siri ya mafanikio

Miaka mitatu iliyopita wakati nimeajiriwa kama mwalimu nilipanga kufanya kazi kwa miaka mitatu wakati nafanya biashara. Katika kipindi hicho nililenga kujiwekea akiba kidogo kidogo ili niweze kukuza biashara yangu kutoka mtandaoni hadi kuwa na duka kubwa.

Niliweka akiba kama nilivyopanga na nilifungua duka dogo ambalo bado sikuridhika nalo.  Niliendelea kuweka akiba hadi kufikia hatua ya kufungua duka kubwa la nguo.

Kila siku nilikuwa najiuliza na kufikiria kwa kina namna nitakavyoweza kujiongeza na kulifikia soko la nyumbani Tanzania na nje ya nchi.

Nilianza kama muuzaji wa bidhaa za rejareja lakini kwa sasa ni mfanyabiashara nayetoa huduma za bidhaa za jumla. Jambo ambalo limekuwa kama chachu kwenye maisha yangu ni kuhakikisha kuwa kila kitu ninachofanya kinasaidia kuleta mabadiliko. Hili jambo linanifariji sana.

Nafarijika sana kuona binti mdogo nawapa na kuwatengeneza fursa watu wenye mitaji midogo kuagiza mizigo nje ya nchi kwa urahisi. Watu hawa wakipata mizigo yao wanafanya biashara nyumbani Tanzania na kubadilisha maisha yao na ya wengine, hili linanipa furaha kubwa kuliko faida ya fedha.

Vipi kuhusu timu ya biashara?

Mimi ndiyo kila kitu huku Uturuki. Kuna wakati unajikuta una majukumu mengi lakini huwa na lazima kufanya kwa wakati na kupumzika hapo baadaye. Kwa upande wa Tanzania nina timu inayojitahidi kupambana katika kufanikisha biashara hii japo kuna wakati natamani ningekuwepo mwenyewe kwa kuwa huwa natamani ningefanya mengi mwenyewe.

Kwa kiasi kikubwa namshukuru Mama yangu kwa meneja mzuri wa biashara yangu Tanzania lakini bila kuwasahau marafiki, ndugu na jamaa kwa sapoti yao.

Biashara au ajira? Chagua moja

Akili yangu ipo tofauti kidogo. Mara nyingi huwa nafikiria vitu hivi viwili yaani ajira na biashara vinaweza kufanywa kwa pamoja. Ajira yako inaweza kukusaidia kupata mtaji wa kuanzisha biashara.

Ukishasimama kwenye biashara unaweza kupumzika ajira na kuendeleza biashara kwa sababu utakuwa na nafasi kubwa ya kufanya mengi kwa uhuru lakini unahitaji zaidi nidhamu ukiwa umejiajiri.

Unajiwekea muda wa biashara kwa nidhamu kubwa kama upo kwenye ajira ili ufikie malengo yako kwa wakati.

Kiukweli nisingependa kubadili chochote kwenye safari yangu kwa sababu namshukuru Mungu kila kitu kimeenda kama nilivyopanga japo si kirahisi lakini angalau naona mwanga sasa kwa kuwa naamini kila siku tunakua na kujifunza kitu kipya.

Msemo au nukuu niipendayo

Kila dola ama Shilingi ina thamani. Huu msemo ni ukweli mtupu na ukiwaza kwa kina hautakuja kudharau hata Shilingi moja.

Ukiweka faida ya dola moja katika kila bidhaa unayoweza kuuza na kupambana uuze kwa idadi kubwa na kwa mzunguko wa haraka basi una uhakika wa kupata kitu.

Ukiweza kuuza bidhaa 1,000 kwa faida ndogo ya dola moja unapata Dola za Marekani 1,000 ndani ya wiki moja ukizidisha kwa wiki nne maana yake ndani ya mwezi una uhakika wa kupata Dola za Marekani 4,000 sawa na takriban Sh9.2 milioni.

Ushauri kwa vijana wenzangu ni kwamba wewe ndo unaweza kuchagua kuanza leo au kusema siku moja nitaanza. Usiwe muoga, kujaribu na kufeli, ni jambo la kujifunza. Unachoona kidogo leo kitakuwa kikubwa hapo baadae ukiweka juhudi.

Kuishi bila ya fikra za ipo siku ni jambo zuri sana ili uweke akiba ya fedha na kufanya mipango ya maendeleo kwa ajili ya maisha yako.

Jambo la msingi hapa ni kwamba usichague biashara kwa sababu jamii itakuonaje na heshima au cheo kisichokuwa na msingi. Siri ya mfuko wako ni akiba yako sio ya jirani yako.

Comment:

  • Najma

    I'm so much impressed! A very humble girl. Thenx for your motivation, its a way to encourage others that they can do it!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.