SHUJAA WA MWEZI
Navy Kenzo, Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva
Na Mwandishi Wetu
Kila binadamu anapenda kufikia malengo kwa kila anachokiwaza kama ndoto yake. Ili kufikia kilele cha mafanikio kuna umuhimu wa kujipanga na kutekeleza fikra alizonazo lakini pia kupambana na changamoto za hapa na pale.
Mwanamuziki Navy Kenzo anaamini kuwa kila mfanyabiashara aliyefanikiwa amepitia changamoto mbalimbali. Nyota huyo wa muziki anafafanua kuwa, si kwamba maisha yake yalikuwa mabaya kabla ya kuanza muziki ila aliamua kuingia katika fani hiyo ili kutimiza ndoto zake. Anakiri kupambana na ugumu wa hapa na pale huku akiwashukuru wazazi wake kwa kutoa mchango mkubwa ili aweze kufika alipo kwa sasa.
“Ugumu mwingi ulitokea kwasasabu ya kutokuwa na uzoefu. Kwahiyo ilibidi kupambana kwa kila hali ili kutimiza malengo tuliyokuwa nayo. Ili kufanikiwa kwa haraka kupitia muziki, unahitaji mtaji mkubwa ili kuufanya katika mitindo yote, kwa maana ya; kufanya video, kutangaza bidhaa yenyewe na jina lako, poromosheni na vitu vingine vingi. Kwakuwa sisi hatukuwa na uwezo huo ilibidi mwenzangu Aiika aajiriwe kwenye kituo cha televisheni ambapo alipata fursa ya kufanya kazi nyingi za uzalishaji ili kupata mtaji. Hatua hiyo ilitusaidia sana,” anasema.
Wakati mwingine kuwa na marafiki wengi ni muhimu katika kupata ushauri. Kwa Navy Kenzo hii ilikuwa tofauti kidogo kwani anadai kuwa, ili kupata walichohitaji waliamua kupunguza idadi ya marafiki, ndugu na jamaa na kupata ushauri kutoka kwa wachache ambao waliwahi kupitia changamoto mbalimbali na wakafanikiwa.
Anaelezea kuwa, kilichowasababisha kufanya muziki kama biashara ni baada ya kugundua kuwa muziki wa enzi hizo ulikuwa katika youtube na itunes kuliko mahala kwingine.
“Enzi hizo mauzo ya muziki ilikuwa sana sana YouTube na itunes ambapo tulikuwa tukipata dolla 10 tunapata motisha ya kuongeza mashabiki zaidi. Wanamuziki wengine kama Vanessa na Joh Makini, walikuwa tayari wameanza kupata malipo kupitia maonesho kadhaa. Yote haya yakatufanya tuone, muziki unaweza kuwa biashara ya maana zaidi,” anaendelea kufafanua
Katika hatua nyingine nyota huyo wa muziki anafafanua kuwa, jambo jingine muhimu ni kupata watendaji wanaotambua majukumu yao ipasavyo na hasa kuielewa kazi ya muziki.
“Ilifikia wakati tukaona tunahitaji wafanyakazi wanaoelewa kazi hii zaidi. Cha msingi tulichojifunza ni kwamba unaweza kuwa na wafanyakazi wazuri ila kama wewe mwenyewe husimamii kwa makini na hujui unachokitaka, hamna kazi ya maana itakayofanyika! Na hii ni mojawapo kati ya changamoto kubwa sana katika mfumo mzima wa uendeshaji biashara, iwe muziki au biashara yoyote! Muhimu zaidi ni kupambana kila mara kupata suluhisho bila kuchoka wala kukata tamaa,” anatanabaisha nyota huyo.
–
Aidha anafafanua zaidi kuwa mbali na muziki wana biashara nyingine kama vile Gold baby products na Navy Kenzo Academy. Hii inachangiwa na umaharufu walioupata. Msanii huyo anaelezea kuwa, licha ya kutaka kufanikiwa kama wasanii bora duniani, wanataka pia kufanikiwa kama wafanyabishara wakubwa.
Nyota hawa wa muziki ambao wamejinyakulia sifa kutokana na kuwa na mtindo wa kipekee, wanasema kuwa, kiasi fulani wanaona wamefikia mafanikio aliyojipangia, kutokana na jitihada binafsi za hapa na pale.
“Tunaweza kusema kuwa kwa upande wa mafanikio tumefikia ni takriban asimilia 35, kwa sababu kuna mambo kadhaa bado hatujayakamilisha ambayo yapo katika ndoto na malengo yetu. Tuko katika mchakato wa kuhakikisha kuwa tunatekeleza kila jambo lililoko katika mpango wetu. Tulianza na muziki, tuna mshukuru Mungu tumefanikiwa katika hilo, ingawa bado tunahitaji kufika mbali zaidi.”
“ Halikadhalika tuna biashara ya bidhaa za watoto ambayo pia imefanikiwa na haitakiwi kuishia hapo. Tunatakiwa kuwahudumia watu wa rika zote! kwahiyo bado tuna kibarua cha kuikuza kampuni na kutoa huduma kwa kila mtu. Kwa mfano, kwa upande wa mpira tuna Shule ya vipaji (Football Academy) ambayo ina mafanikio makubwa sana, hasa kutoa vijana katika timu za taifa na katika vilabu vya nje ya nchi. Lengo sio kuishia hapo, tunahitaji kuendelea kuibua vipaji vingi vya mpira kuvipeleka nje ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Ukijumuisha yote haya utaona kuwa tumefikia asilimia 35,” anamalizia kufafanua.
“Wito na ushauri wetu kwa vijana, ni kuanza kwa kujiwekea malengo binafsi. Huwezi kua kijana wa miaka 25, huna malengo au picha kichwani ya mafanikio unayotaka kuyafikia kabla ya miaka 35 au 40. Hutoweza kufanikiwa bila kujua unataka mafanikio ya aina na kiasi gani, kisha kua na mkakati wa kuyafikia malengo hayo!” aliongeza Navykenzo
“Kubwa zaidi ni kua na mwenza mwenye malengo ya kufanana na yako, hii itawasaidia sana kufika mnapoelekea bila kupoteza muelekeo njiani kutokana na kupishana malengo na mtizamo wa maisha. Aika ni mwenza mwenye malengo makubwa na msimamo sana! Pia bidii na utulivu wa akili, naweza kusema kwa asilimia kubwa sana, amesaidia sisi kama familia kufikia mafanikio tuliyo yafikia. Pia ana nipa confidene kua hiyo asilimia 65 iliyobaki, tutaifikia pia! Kijana mwenye ndoto kubwa, usipuuze umuhimu wa kupata mwenza sahihi ili ufukie malengo yako haraka!” alimaliza nyota huyo.
Aika pia alihimiza sana umuhimu wa kijana wa kike kujitambua na kujua thamani yake, kujiwekea malengo makubwa na kujiamini anaweza kufikia malengo hayo. Kwa Aika, kua na mwenza bora imekua chachu ya maendeleo na kujenga familia bora yenye misingi na viwango tofauti na wengi. Bidii katika kazi, kutoyumbishwa na starehe au vizingiti visivyokua na msingi ni baadhi ya misimamo aliyojiwekea Aika na kuona mafanikio makubwa katika kuiishi misisamo hiyo.
Hakika, Navykenzo na Aika ni vijana wa kuigwa kutokana na mafanikio waliyokua nayo hasa kama familia na kama kundi la muziki. Ni moja kati ya wasanii wachache wenye nyumba kali, biashara zinazo waingizia kipato zaidi ya muziki na vijana wenye bidii bila kuchoka tangu walipoanza muziki na biashara hadi sasa! Siri yao kama walivyoeleza ni kua na Malengo, mwenza bora na mwenye bidii na kuongeza vyanzo vya mapato kila mwaka, kadiri unavyoweza!
Leave a Reply