TEL: +255 752 920 592

SAFARI YANGU KUFIKIA UHURU WA KIFEDHA

By Nancy Sumari, Founder Jenga Hub & MD Bongo5 Media Group

Wengi wamekuwa wakinisikia ama kuniona katika harakati za kuhamasisha masuala lukuki yenye manufaa kwa jamii yetu ya Tanzania. 

Licha ya kuwa mmoja ya wanahamasishaji wa masuala hayo ya kijamii yakiwemo masuala ya kifedha, leo ningependa kuwamegea kidogo manufaa ya safari yangu binafsi ya Uhuru wa Kifedha. Ni watu wachache hueleza siri hizi binafsi kwa jamii ili ijifunze na kukata minyororo iliyowafunga hasa inayohusu fedha. 

Safari hiyo, iliyonifanya niuone ulimwengu mpya katika masuala ya fedha, niliianza baada ya kutambua malengo yangu na ndoto zangu binafsi za kimafanikio na kuamua kuzifanyia kazi. 

Hata hivyo, safari hiyo si lele mama bila mipango. Awali nilijaribu mbinu mbalimbali zikiwemo zilizofeli na kufanikiwa. Sikukata tamaa. Kila siku nilindelea kujielimisha na kujaribu zaidi na zaidi. Pamoja na vikwazo hivyo, kwa sasa naweza kutembea kifua mbele na kuwaeleza kuwa nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika safari yangu hii. 

Nilifanya mambo gani ili kufikia kilele hicho cha mafanikio? Leo ningependa ‘kushare’ (kukupatia) baadhi ya mbinu zinazoweza kukusaida unapoanza safari yako ya uhuru wa kifedha.

Kujiwekea mpango mkakati thabiti wa matumizi 

Baada ya kusogea kiumri, niligundua kwamba ninahitaji mkakati maalum wa jinsi ninavyotumia fedha zangu. Katika kujielimisha kuhusu hili, niliigundua ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuyagawa majukumu ya kifedha kwa makundi na hatimaye kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima au umuhimu sana. Kupitia mgawanyo huu nilibaini kuwa nitaongeza kiasi cha fedha ninachookoa kutokana na matumizi yasiyo ya lazima na pia kujenga nidhamu ya Pesa. Hivyo, nikaanza na hili, kuhakikisha kila kitu kwenye Mipango yangu kinatimia.

2. Kujiwekea akiba ya dharura

Jambo la pili muhimu nililofanya ni kujiwekea akiba ya dharura. Wataalamu wa usimamizi wa fedha wanasema ni muhimu kwa kila mmoja kuhakikisha kwamba anajiwekea akiba ya dharura ya mwaka mmoja na ikiwezekana zaidi ya mwaka. 

Akiba hii inatakiwa ilingane na kiasi chako cha matumizi ya mwezi na kuzidisha kwa miezi 12. Wataalam wengi wa masuala ya kifedha wanashauri kutokukosa akiba ya dharura ili kuhakikisha kuwa hautetereki katika maisha yako, pale inapotokea dharura. Kwa mfano, kama matumizi yangu ya mwezi ni Sh1, 000,000 basi akiba yangu ya dharura itakua Sh12,000,000. Kujenga akaunti hii, nilitumia karibu miezi sita kutimiza.

3. Wekeza, wekeza, wekeza 

Ili kukuza kipato chako cha sasa na hasa cha baadaye, huna budi kuwekeza kwenye mali zenye kuzalisha au miradi ambayo thamani yake na mrejesho wake huongezeka. 

Mifano mizuri ya mali au uwekezaji huo ni kuwekeza katika ardhi, ununuzi wa hati fungani za benki (bonds), hisa za kampuni mbalimbali zilizopo katika soko la hisa, nyumba, biashara uliyoitafiti kujiridhisha nayo na kadhalika.

Hadi sasa mimi ninaendelea kuwekeza kila mwezi na kila mwaka kulingana na ukuaji wa mapato yangu. Aina ya uwekezaji ninaoupenda na kuonyesha mafanikio kwangu ni biashara katika sekta ya teknolojia pamoja na kutoa elimu. Faida ninazo pata kutokana na biashara hizi, natumia kukuza au kuongeza biashara na hatimaye, kukuza faida na kipato changu zaidi na zaidi. Kwa sasa, najielelimisha kuhusu uwekezaji wa ardhi na kununua hisa, nitakapofuzu basi nitahamishia bidii zangu za kuwekeza katika mambo hayo.

4. Pata mshauri wa masuala ya fedha

Katika ulimwengu huu yatupasa kupata mshauri wa fedha kama tulivyo na daktari wa kututibu. Ingawa kufanya utafiti na kujielimisha kuhusu masuala ya fedha ni muhimu, kuwa na mtaalamu wa masuala ya kifedha kuna faida zake. 

Binafsi nimepata ushauri mkubwa kutoka kwa wataalamu wa fedha kutoka benki yangu ya NMB. Kuna wataalamu, waelewa na wepesi kutoa maelekezo na pia ushauri wa masuala ya kifedha kutokana na hali yako ya kiuchumi na namna ya kuongeza ufanisi wa fursa za kifedha. Zingatia wanachoshauri na uliza maswali mengi uwezavyo ili kujipatia uelewa zaidi.

5. Tumia Teknolojia (Mipango App)

Teknolojia ikitumiwa kwa njia sahihi, inasaidia kuongeza ufanisi wa hali ya juu hususan kwa masuala ya kifedha. Application (programu) au tovuti kama hii ya Mipango App imejikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya maendeleo. 

Huu ni uwanja wa kujipatia ushauri na mafunzo ya usimamizi binafsi wa kifedha kutoka kwa wataalamu mbalimbali na watu mashuhuri waliofanikiwa katika usimamizi wa fedha na malengo ya maendeleo. Kupitia Mipango, utajifunza ujasiriamali, kujiwekea mikakati na kusimamia mikakati yako. 

Karibu uijaribu leo, hakika ​​hautojutia.

Mbinu hizi tano zimeleta mafanikio makubwa katika maisha yangu na mkakati wangu kufikia uhuru wa kifedha. Zinaweza kukusaidia wewe katika mkakati wako au kuwa chachu ya kuanza mkakati wako binafsi. 

Mwisho kabisa, nakusihi wewe kama kijana, wa kike au wa kiume, kufanya maamuzi ya kuyatambua malengo yako na kuanza kuyafanyia kazi kwa wakati kabla ya mwili kuchoka. 

Kama una ndoto na malengo ya kuwa na biashara au kipato chenye ukubwa fulani, kaa chini ujue biashara hiyo au kipato hicho na kujiwekea mikakati ya muda mfupi na muda mrefu itakayokuwezesha kufikia malengo hayo. 

Pia, changamoto zinapokujia katika safari yako ya uhuru wa kifedha, usikate tamaa! Jitahidi kujiweka karibu na watu wenye malengo makubwa zaidi au sawa na yako, ili wakupe moyo na mbinu, pale utakapo hitaji.

Utaweza, Unaweza, Amua!

Comment:

  • Athuman Nchullah

    Hongereni kwa kazi nzuri mnayoifanya, ninajifunza mengi kupitia tovuti yenu. Hivi karibuni nimeona app ya mipango, lakini nimeona inahitaji maboresho kidogo. Mfano inajumlisha mapato na matumizi badala ya kutoa. Pia haina sehemu ya ku edit malengo baada ya kuyaweka. Mi nashauri kuwepo na sehemu ya ku edit malengo mtu aliyojiwekea ili kurahisisha upanukaji wa mawazo. Pia nashauri kuwe na uwezo wa kupata ripoti kwa mfumo wa PDF, mnaweka weka gharama kidogo katika app ili kusaidia na kuwezesha maboresho ya mara kwa mara. Asanteni mno

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.