TEL: +255 752 920 592

PANGA KUSTAAFU AU JIKUTE UMESTAAFU!

Kupanga kustaafu ni kuweka malengo ya kustaafu na utaratibu madhubuti wa jinsi ya kutimiza malengo hayo katika kipindi fulani. Katika maana hii tunapata mambo makuu matatu muhimu ya kuzingatia; kwanza ni kuweka malengo ya kustaafu, kisha ni mikakati ya kuyafikia hayo malengo na tatu ni muda wa mpango wa kustaafu.

 • Malengo ya kustaafu yanajumuisha:
  • Muda wa kustaafu, mfano; mwaka gani, kwa hiari au kwa mujibu wa sheria.
  • Vyanzo vya kipato baada ya kustaafu.
  • Makazi yako baada ya kustaafu n.k.
 • Mikakati ya kuyafikia malengo ya kustaafu ni pamoja na:
  • Kuwa na mpango wa muda mfupi na muda mrefu.
  • Kuanza mapema maandalizi i.e kipato mbadala, makazi, mtindo wa maisha n.k
  • Kuwashirikisha wataalam, wabobezi na wazoefu.
  • Kuainisha na kuwa na rasilimali za kutekeleza mpango.
 • Muda wa mpango unaweza kuwa:
  • Utekelezaji wa mpango.
  • Nini kianze na nini kifuatie.
  • Muda wa tathmini ya mpango n.k.

Kuna umuhimu gani wa kupanga kustaafu?

Kupanga kustaafu humsaidia mwajiriwa kufanya maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu. Ni muhimu kuwa na picha ya maisha ya kustaafu mapema. Mwaka 2018 Benki ya Dunia ilitoa takwimu zilizoonesha kuwa wastani wa kiwango cha umri wa kuishi nchini Tanzania kiliongezeka kutoka miaka 58.5 mwaka 2010 hadi miaka 65 kwa mwaka 2018. Ongezeko hili linadhihirisha umuhimu wa kupanga kustaafu kama sehemu ya maandalizi ya maisha baada ya kustaafu. Kupanga kustaafu humsaidia mwajiriwa kufanikisha mambo kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na: 

 • Kuainisha aina gani ya maisha aishi baada ya kustaafu ajira.
 • Kuepuka au kujiandaa na changamoto zinazotokana na kustaafu.
 • Kumsaidia mwajiriwa kubaini fursa zitokanazo na kustaafu na kuzitumia vema.
 • Kupunguza hatari zinazoweza kutokana na utegemezi mkubwa wa mafao ya kustaafu.
 • Kupunguza utegemezi na changamoto za kutunzwa au kulelewa na familia

Lini mwajiriwa apange kustaafu?

Mwajiriwa anaweza kupanga kustaafu katika kipindi chochote cha ajira. Hata hivyo ni vema kuwa na mpango wa kustaafu katika hatua za mwanzo za ajira yake. Kwa vile mpango wa kustaafu huweza kubadilika siku hadi siku kulingana na mazingira na mahitaji ya mwajiriwa basi ni vema kuandaa mipango yake ya kustaafu mapema. Lakini hata mwajiriwa anayekaribia kustaafu au ambaye amestaafu bado anaweza kuandaa mpango wake wa kustaafu na ukawa wenye msaada mkubwa sana. Hivyo basi ni vema tukisema kuwa kuandaa mpango wa kustaafu ni suala la wakati wote kwa mwajiriwa, hakuna kuwahi wala hakuna kuchelewa.

Imeandikwa na,

Anselm Namala,

Retirement Planning Consultant,

Mpingo Business Consultants, Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.