TEL: +255 752 920 592

Mambo 8 ya kufanya ili kuvunja akili ya kimasikini

Mazingira tuliyokulia huongoza au huamua tutakua watu wa aina gani pindi tunapokuwa watu wazima na kujitegemea. Kama ulikulia kwenye mazingira ya kujiamini na kufanyakazi kwa bidi, uwezekano mkubwa, utakua mtu mwenye kujiamini na kufanya kazi kwa bidi. Kama umekulia kwenye familia yenye watu wavivu na wasio jiamini, uwezekano mkubwa utakua hivyo hivyo.

Akili zetu hujifunza kwa kuona, kusikia na kurudia jambo mara kwa mara (mazoea).

Akili inapojifunza jambo, huliweka kumbukumbu kwenye fahamu zako na kukuwezesha kufanya jambo hilo wakati ujao bila kutumia ufahamu wako wote. Ndio maana tunajifunza kuendesha gari, kulima, kutembea nk. Na bila kutumia akili au ufahamu wetu wote, tunaweza kufanya mambo haya wakati wowote.

Ndivyo ilivyo kwenye masuala ya fedha, kazi na kujiamini. Yale tuliyoona na kujifunza hujiandika akilini mwetu na kujikuta tunafanya maamuzi mabaya ya fedha na maisha bila kuamua kufanya hivyo kwa ufahamu wetu wote.

Kama wewe ni miongoni mwa waliokuwa kwenye mazingira ya kuamini ni masikini hivyo huwezi kuwa tajiri, au hustahili kujiamini au kuwa na ndoto kubwa, au pesa na matajiri ni watu wabaya, basi chukua hatua sasa ijaze akili yako Imani mpya, amini unaweza kufanikiwa na hata kuwa tajiri hata kama mazingira yako ni ya kimaskini.

1. Tengeneza urafiki na watu wenye mawazo chanya

Wanasema, mtoto hujifunza kwa anachoona zaidi ya anachoambiwa. Hivyo hatua ya kwanza ya kuondoa mawazo ya kimaskini ni kutafuta marafiki wenye kuamini kuwa wanaweza, wanastahili kufanikiwa na wanafanya jitihada za kufanikiwa. Kwa kuzungukwa na watu wa aina hii, utajikuta umeamini wanachoamini, Pia kwa kuona jitihada zao na matokeo yao, utajikuta na wewe unajiamini na kufanya jitihada kufanikiwa. Epuka marafiki, ndugu na jamaa wanaopenda kulalamika kila mara, wanaoamini kuwa mafanikio ni kwa ajili ya matajiri tu na kwamba watu wenye hali duni hawawezi kuwa matajiri pia, wenye kuongelea vibaya waliofanikiwa nk.

2. Acha Kuongea lugha ya kimasikini

Hatua ya pili ya kukuwezesha kuvunja mawazo ya kimasikini, ni kuepuka kuongea lugha za masikini. Mfano ‘tumeumbiwa shida’ , ‘maisha magumu sana’, ‘cha muhimu uhai’, na misemo mingine kama hiyo. Falsafa ya Sheria ya kuvutia ni imani kwamba mawazo mazuri au hasi huleta matukio mazuri au mabaya katika maisha ya mtu. Unachowaza na kuongea ndicho kitakachotokea. Hata kwenye vitabu vya dini, imeandikwa ulimi huumba, hivyo tumia mdomo wako kujiumbia mafanikio, na si vinginevyo.

3. Tengeneza sentensi chanya zinazo kuhusu na kujisemea kila siku

Hatua ya tatu ni kuchagua maneno matatu hadi matano chanya ya kujisemea kila siku ili kufundisha akili yako kuamini mtizamo mpya kuhusu wewe. Hii ni mbinu inayotumika na wenzetu katika nchi zilizoendelea ambao hujisemea sentensi chanya tangu wanapokua na umri mdogo sana. Mfano, ‘mimi nina akili, bahati na nitafanikiwa sana!’ kisha sema maneno haya kila siku asubuhi kabla ya kuanza shughuli zako. Mwanzoni utaona kama unajidanganya, hadi siku utajikuta akili yako imeamini kabisa maneno haya na kuyaishi na hivyo, kuvutia mafaniko kwenye maisha yako.

4. Badili mtazamo wako juu ya utajiri/ matajiri

Hakuna watu wanaowachukia watu walio na mafanikio, kama wale walio chini yao. Na huo ndiyo mzigo unaowafanya wasiweze kufikia mafanikio walionayo ya utajiri. Watu wenye mawazo ya kimaskini wamejawa uchungu unaowafanya kuwachukia au kuwaongelea vibaya wenye mafaniko. Wengi husema maneno kama ‘matajiri wana roho mbaya’, ‘matajiri hawana furaha’, ‘kafanikiwa kwa kutoa kafara’, ;hizo mali sio zake’ nk. Kuamini hivi kuna kufanya kuchukia mafanikio, na huwezi kupata unachokitaka.
Amini kuwa, unaweza kuwa tajiri na ukawa na roho nzuri, Amani kwenye familia yako na furaha tele. Hata hivyo hata masikini hupata matatizo na hukosa furaha pia, usidanganyike na maneno ya mkosaji.

5. Fanya zoezi la shukrani

Hatua ya tano ni kutambua Baraka ulizonazo au mazuri yaliyoko kwenye maisha yako, yafurahie na mshukuru Muumba wako kwa Baraka alizokupa. Hata kama hujafanikiwa, kuna mazuri kwenye maisha yako, una marafiki wanaokupenda, ndugu na familia inayokujali, mahali pa kulala na kuishi, ajira nk. Kutambua mazuri haya kutakufanya uwe mtu mwenye furaha, sio uchungu na chuki kila wakati. Shauku yako itakupa nguvu ya kuendelea kupambana kutafuta mazuri zaidi unayotamani kuwa nayo, mtu mwenye chuki na hasira huzuia hata akili yake kuona fursa pamoja na kuwa na utayari wa kujaribu.

6. Jifunze kutuliza akili yako
Moja ya mzigo mkubwa wa masikini ni hofu! Hofu hukuzuia kuiendea fursa kwa kujiamini katika yale uyafanyayo au unayotaka kufanya. Watu wenye mafanikio sio kwamba hawapitii mazingira magumu, yanayowapelekea kuvunjika moyo wakati wa shughuli za utafutaji au maisha kwa ujuml. La hasha, wanapitia ila wanao uwezo wakuziongoza akili zao kufanya yale wanayotakiwa kufanya kwa ujasiri.

Ili uweze kutuliza akili yako, jiwekee ratiba za kupumzika katika mazingira mazuri, kukaa na marafiki na kucheka nk. Jiwekee bajeti kidogo ya kusafiri, hata mkoani au ufukwe uliopo karibu nawe ili kutuliza akili na kuipumzisha mara kwa mara. Akili iliyotulia, ina mazingira mazuri ya ubunifu na mawazo bingwa!

7. Panga Mpango wa kufikia Malengo yako

Hatua ya saba ni kujiwekea malengo binafsi ya mendeleo. Hakuna kitu kibaya kama kuishi bila malengo, yani unaishi tu ilimradi….huwezi fika popote maana huelekei popote. Tafuta siku, kaa na ujiwekee malengo ya muda mfupi na ya muda mrefu ya maisha yako, kisha andaa mkakati wa kuyafikia malengo hayo. Wengi hufanya zoezi hili mwanzo wa mwaka, na kujiwekea malengo ya mwaka mzima na mkakati wa kuyafikia. Kama hujafanya hivyo, hujachelewa, anza na malengo ya miezi mitatu, sita hadi uweze ya mwaka. Hakikisha malengo yako yanafikika ila usiwe muongo kujiwekea malengo nje kidogo ya uwezo wako. Hakikisha mwisho wa hiyo miezi mitatu/ sita au mwaka, unakaa na kujitathimini ili ujue namna ya kujiboresha.

8. Jipende, Jijali
Hatua ya mwisho ni kujipenda na kujijali. Watu wanaojipenda, hula vizuri, huvaa vizuri na kutafuta mazingira ya kufurahia maisha. Usiruhusu maisha ya kutafuta yakakufanya ujisahau kabisa. Unatakiwa kuwa na afya nzuri, nguvu na furaha ili uweze kuzalisha au kufanya kazi zaidi. Mtu mlevi na mchafu, zaidi ya kukosa muda wa kujijenga, havutii kukaa na watu chanya, huzungukwa na watu wenye tabia kama zake na kujididmiza zaidi.

Nakutakia kheri katika kubadili mawazo/ akili ya kimasikini na kuingia katika ulimwengu wa kujiamini, malengo makubwa na mikakati ya kuyafikia malengo yako!

Lilian Makoi, Muanzilishi, Mipango Fintech Ltd

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.