Mambo matano gumzo bajeti 2021/22
Mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22 yamesomwa leo tarehe 10 Juni, 2021 bungeni huku mambo matano yakionekana kugusa zaidi wananchi na kuzua mijadala kwenye mitandao ya kijamii.
Suala la kwanza Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Mwigulu Nchemba amesema serikali imependekeza kufanyaka marekebisho kwenye sheria ya kodi ya majengo, sura 289 ili ukusanyaji wa kodi ya majengo ufanyike kwa kutumia mfumo wa ununuzi na utumiaji wa umeme kupitia mashine za Luku.
Dkt. Nchemba amesema kila mita ya umeme ina uhusiano na mmiliki wa jengo au mtumiaji wa mita, na kwa kuwa sheria ya kodi ya majengo inataka kodi hiyo ikusanywe kwa mmiliki au mtumiaji wa jengo, hivyo, napendekeza kodi ya majengo ya kiwango cha shilingi 1,000 kwa mwezi kwenye nyumba za kawaida zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme yaani luku.
“Serikali imependekeza kiwango cha shilingi 5,000 kwa mwezi kwa kila ghorofa au apatment zenye mita moja na itakatwa kwenye luku na itaweka utaratibu kwa nyumba za kawaida na ghorofa zinazochangia mita moja na mita Zaidi ta moja,”
Eneo jingine ambalo limegusiwa ni kuongeza ushuru wa barabara kwa Shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli, kufanya marekebisho ya kifungu cha 4 A (a) cha sheria ili kuelekeza fedha zitakazokusanywa kutokana na ongezeko la ushuru wa barabara na mafuta la Shilingi 100 kwa aina zote za mafuta ziwe kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za vijijini kupitia Tarura.
Tatu ni, Serikali imependekeza kutoza tozo ya shillingi 10 hadi Shilingi 10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa. Kiasi cha tozo kinatofautiana kulingana na thamani ya muamala wa fedha unaotumwa au kutolewa. Pendekezo hili litaongeza mapato ya Serikali kiasi cha Shillingi milioni 1,254,406.14 hii pia inaenda sambamba na suala la ukataji wa Shilingi 10 hadi 200 kwa laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji, hili litapelekea kuongeza mapato ya Serikali kiasi cha shillingi milioni 396,306.0
Nne, Dkt. Nchema amesema ni kupunguza adhabu zinazotolewa chini ya Sheria ya Usalama Barabarani sura 168 kwa makosa ya pikipiki na bajaji kutoka Shilingi 30,000 za sasa hadi Shilingi 10,000 kwa kosa moja. Lengo la hatua hii ni kuweka adhabu kwa kuzingatia uwezo wa kulipa. Aidha, adhabu kwa makosa mengine ya vyombo vya moto zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria zinaendelea kubaki kama ilivyo sasa.
Mwisho ni, kupunguzwa ushuru wa bidhaa kwenye bia zinazotengenezwa kwa kutumia shayiri iliyozalishwa hapa nchini kutoka Shilingi 765 kwa lita za sasa hadi Shilingi 620 kwa lita, lengo la mapendekezo haya ni kuchochea kilimo cha shayiri hapa nchini.
Mijadala mbalimbali imeibuka kwenye mitandao ya kijamii huku pande mbalimbali zikieleza unafuu na maumivu yaliyopo kwenye bajeti hiyo hususani makato ya adhabu ya makosa barabarani kwa waendesha bajaji na pikipiki.
Leave a Reply