TEL: +255 752 920 592

KUFELI SIO KIGEZO CHA KUSHINDWA

John Maxwell mwandishi nguli wa vitabu vya uongozi aliwahi kusema “Mtu aliyeshindwa mara mara nyingi anajua mambo mengi kuliko mtu ambaye hajawahi kushindwa kabisa”.

Inawezekana umeshindwa kwenye kitu unachofanya na kupoteza matumaini ya kuwa mshindi tena kwenye maisha yako; hofu ya kufeli imetawala maisha yako kuona huwezi tena lakini kumbuka ushindi upo ndani ya kushindwa.

Unaweza kufeli mara nyingi kwenye mambo tofauti tofauti kwenye maisha yako, lakini usikubali kuona ndio mwisho wa wewe kufanikiwa na kupiga hatua sehemu ambayo upo kwenda hatua za juu zaidi, inawezekana na ipo ndani ya uwezo wako.

Je, unamfahamu Thomas Edison mwanasayansi ambaye alifeli mara 999 kwenye jaribio lake la kugundua balbu ya umeme? Lakini mara ya 1000, jaribo la ugunduzi wa umeme likafanikiwa na kuwa mgunduzi wa kwanza wa balbu ya umeme ambayo tunaitumia sasa kwenye maisha yetu ya kila siku! Swali ni kwamba, upo tayari kuthubutu kujaribu kama Thomas Edison kwenye malengo yako pamoja na harakati zako?

Je, unajua tajiri mkubwa kutoka nchi ya China Jack Ma alifeli kwenye maombi ya kazi kwenye migahawa maarufu ulimwenguni kama KFC na pia alifeli zaidi ya mara tano kwenye maombi ya kujiunga kwenye chuo kikuu cha Havard Marekani? Jack Ma alifeli mara nyingi lakini hakukubali hofu ya kufeli kuwa tiketi ya Kushindwa; baada ya muda ndio ikawa nafasi ya kuwa mwanzilishi wa soko kubwa la mtandaoni la Alibaba, Je upo teyari KUTHUBUTU kujaribu pasipo kujali umefeli mara ngapi kwenye maisha yako?

Je, biashara unayofanya imefeli? umepata hasara na kuona hustahili kuwa mfanyabiashara tena kwenye biashara yako?

Je, maisha ni magumu kiasi umepoteza matumaini na kuona bora ukate tamaa kwenye maisha yako?

Je, harakati haziendi kabisa kila siku huoni matokeo kwenye harakati zako?

Kumbuka kukata tamaa haifanyi maisha kuwa rahisi, nafasi pekee ni kujifunza kwenye kufeli kwako na kuona sehemu gani ulikosea ufanyie marekebisho gani ili mbeleni usifeli kwa namna ile ile. Usiruhusu hofu ya kufeli kukufanya kuona ndio mwisho, bali ona kufeli kwako ni daraja na darasa kuelekea kilele cha ushindi.

Mwanafalsafa maarufu Plato aliwahi kusema “Watu wanachukia sana watu wanao zungumza ukweli mchungu” ukweli ni kwamba unaweza kufeli kabla ya kuanza au ukafeli baada ya kuanza, lakini Kamwe usikubali kukata tamaa kuwa huwezi kufanikiwa kwenye maisha yako pasipo kujali umefeli mara ngapi.

Ushindi umejificha ndani ya siri kubwa mbili ambazo ukizijua moja kwa moja utaweza kuwa mshindi, muhimu kuyafanyia kazi siri hizi;-

  1. Nini unataka kwenye maisha yako? Kila mtu anataka kuwa mshindi, Je unajua kwanini unataka kuwa mshindi kwenye maisha yako? Ukijua unachotaka kwenye maisha yako ni hatua Kubwa ya kuelekea kilele cha ushindi lakini usipojua kwanini unataka kuwa mshindi kuna asilimia kuwa ya kutokuwa mshindi kabisa kwenye kitu unachofanya.
    Kujua nini unataka inakupa mamlaka na muongozo wa nini ufanye ili uweze kushinda, pasipo kujali utafeli mara ngapi kwenye kitu hicho. Mwisho wa siku lazima uwe mshindi kwenye kitu unachofanya. Mfano timu yenye kutaka kushinda ubingwa ni lazima wachukue hatua ya kujiandaa vizuri kwa ajili ya mshindano ili wawe mabingwa pasipo kujali katikati ya mshindano watapoteza mchezo. Lengo lao ni kuwa mabingwa. Tazama timu za mpira, wana michezo, waigizaji, wafanyabiashara, utaona ukweli kwenye siri hii ya kwanza.
  2. Kulipa gharama ya Ushindi. Baada ya kujua nini unataka ili uwe mshindi kwenye kitu unachofanya, swali ni kwamba Je, upo teyari kulipa gharama ya kupata ushindi kwenye kitu unachotaka? Hapa ndio tofauti ya watu wenye kutaka ushindi na wanalipa gharama ili wapate ushindi huo na wale ambao wanataka ushindi kwa kusema lakini hawapo teyari kulipa gharama ili wapate ushindi kwenye kile unachofanya.
    Kulipa gharama ni pamoja muda, fedha, nguvu, uvumilivu, uthubutu, uaminifu, ujasiri n.k kupata matokeo ni pamoja na uteyari wa kulipa gharama kwenye kitu ambacho unataka kwenye maisha yako na kupata mabadiliko kwenye kitu hicho hatimaye kupata ushindi. Mfano, ili uweze kua mwanamichezo mkubwa ni lazima ulipe gharama ya kufanya mazoezi kila siku, kunapata maumivu pasipo kujali unajisikia au hujisikii ili uwe mshindi kwenye eneo la michezo.

Siri hizi mbili ambazo ni muongozo kueleka kilele cha ushindi kwenye kitu unachofanya, kabla ya kuendelea, thubutu kwa kuandika nini unataka kwenye maisha yako na kwanini unataka kitokee kwenye maisha yako na gharama zipi utaingia ili upate unachotaka kwenye maisha yako.

Nepeleon Hill mwandishi wa Kitabu cha Think and Grow Rich aliwahi kusema “Mshindi kamwe haachi, na muachaji kamwe hashindi” haijalishi umefeli mara ngapi usikubali kuacha wala kukata tamaa kwenye kitu unachofanya, kuwa king’ang’anizi mpaka mwisho wa kitu hicho.

Kufeli kwenye maisha kupo na ukifeli tambua umejaribu kitu kipya tofauti na mazoea na kutoka kwenye eneo la kuridhika (Comfort zone) na kufanya kitu kipya ambacho baada ya muda utapata matokeo na ushindi endapo tu utajifunza kupitia kufeli kwako na kufeli kwa watu wengine.

Ukiona hujawahi kufeli kwenye maisha yako basi unafanya vitu rahisi au vitu ambavyo umezoea kufanya na hupati changamoto yeyote. Kukua ni pamoja na kukutana na changamoto mpya na ukifeli utajua ufanye nini ili ugeuze changamoto hizo kuwa fursa ya wewe kushinda na sio kushindwa.

Usiruhusu hofu ya kufeli kuwa kikwazo cha wewe kusonga mbele kwenye maisha yako lakini unapaswa kujenga uwezo wa kushinda hofu ya kufeli kwa kuongeza uwezo wa kujiamini (Pitia makala ya shinda uoga wako ujenge maisha yako kwenye blog yetu).

Kufanya makosa kwenye safari ya kuelekea kilele cha ushindi ni kawaida na ni sehemu ya maisha hivyo huna sababu ya kujutia kwanini umekosea na kutumia muda mwingi kufikiria kwanini umekosea, bali jifunze kupitia makosa yako kisha songa mbele na sio kuwaza makosa yako ya nyuma kwenye leo yako; wakati ndio sasa ili ujenge kesho yako njema ni kuanza sasa kuchukua hatua.

Comment:

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.