TEL: +255 752 920 592

JINSI YA KUJENGA TABIA YA KUWEKA AKIBA NA UWEKEZAJI.

Dave Ramsey mwandishi wa vitabu vya fedha aliwahi kusema “Asilimia 80% ya tabia zetu kuhuathiri kufanikiwa au kutofanikiwa kwenye eneo la fedha na asilimia 20% tu huchangiwa na maarifa, ujuzi na uzoefu kuhusu fedha” hitaji la kila mtu ni fedha na afya ndio maana kila siku watu wanapambana ili kupata fedha ili kuendesha maisha yao ya kila siku.

Kupata fedha sio rahisi lakini changamoto kubwa zaidi ni; kuweka, kutunza na kuzalisha fedha. Hapa ndio tofauti ya matajiri na maskini inapokuja, matajiri wanapata fedha kisha wanatunza hatimae wanawekeza ndio maana wanapata faida lakini maskini anapata fedha kisha anatumia pasipo kufanya uwekezaji wowote wenye kuzalisha fedha au faida kupitia fedha zake.

Hakuna ambaye hajui faida ya kuweka akiba na kuwekeza.

Bahati mbaya mafundisho mengi kuhusu elimu ya fedha yanafundisha sheria na kanuni za kuweka akiba na kuwekeza lakini yanasahau kitu kikubwa zaidi, namna ya kujenga tabia ya kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa faida.

Ndio unajua faida ya kuweka akiba, Je una akiba kiasi gani umeweka hadi sasa?

Ndio unajua faida ya uwekezaji, Je umewekeza kwenye maeneo mangapi hadi sasa?

Hivyo maarifa kuhusu elimu ya fedha hayatoshi kukufanya uweze kuelekea uhuru wa kifedha kwa kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa faida.

Tabia ndio ina nafasi kubwa katika kukufanya wewe uweze kuelekea uhuru wa kifedha.

Tabia ni nini?

Tabia, Ni kitendo cha kufanya jambo fulani kwa kujirudia rudia na kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku, hadi kufanya jambo hilo pasipo kujiuliza ufanye au usifanye lakini utafanya.

Umeshawahi kusikia mtu anasema nikipata kiasi fulani nitaweka akiba kiwango fulani lakini akipata tu kiasi hicho anasahau kabisa kuweka akiba na kufanya matumizi mengine na fedha ukiisha ndio anakumbuka kuwa hajaweka akiba kabisa; ukimtazama mtu huyu sio hajui faida ya kuweka akiba lakini tabia ya kuweka akiba hana, ndio maana ya msemo wa Kiswahili unaosema “Pata fedha tujue tabia yako”. Tabia ina nafasi kubwa mno katika kufanikiwa au kutofanikiwa kwenye eneo la fedha.

Kuna tabia ambazo unazo ndizo zinakukwamisha kabisa wewe kufanikiwa kifedha na kushindwa kuweka akiba kabisa, wala kufanya uwekezaji wowote kwenye maisha yako.
Inawezekana tabia ambayo unayo imetokana na sababu zifuatazo;

  1. Malezi ambayo umekulia
    Hujajengewa kabisa utamaduni wa kuweka akiba toka ukiwa mdogo mpaka unakua, unaona kawaida na maisha yanaendelea kila siku pasipo kuweka akiba wala kufanya uwekezaji wa muda mrefu.
  2. Mtazamo
    Unaamini watu ambao wanapaswa kuweka akiba na kufanya uwezaji ni wenye kipato kikubwa sana, kumbe ni mtazamo ambao sio sahihi.
  3. Mazingira ambayo umekulia
    Hujaona wala hujapata uzoefu wowote kuhusu kuweka akiba na kufanya uwekezaji kwenye mazingira ambayo umekulia, umeona wanaokuzunguka wakipata fedha wanatumia kwenye matumizi mengine wala hawaongelei kuhusu akiba na kufanya uwekezaji.
  4. Kipato chako
    Unaamini kipato ambacho unacho hakitoshi kabisa wewe kuweka akiba ya fedha zako wala kufanya uwekezaji wowote wa faida, unaamini kipato ambacho unacho ni kwa ajili ya matumizi ya kila siku ili maisha yako yaendelee kusonga.
  5. Kuamini katika utajiri wa bahati/ haraka
    Umesikia kuhusu bahati nasibu, inawekezana unaamini ukitumia fedha ambayo ulipaswa kuweka akiba na kufanya uwekezaji ukatumia kwenye michezo ya bahati, utapata fedha nyingi na matumaini ya kupata fedha nyingi. Mfano kucheza Kamari unapoteza fedha nyingi lakini bado matumaini utapata kwa kuona wengine wanapata.

Baadhi ya sababu ambazo nimetaja inaweza kupelekea kupoteza fedha na kuwa na tabia ya kutokuweka akiba na kufanya uwekezaji.

Mpaka hapa unasema, ‘nataka niwe na tabia ya Kuweka akiba na kufanya uwekezaji’. Kusema ni rahisi lakini kuwa na tabia hizi ni mchakato ambao watu wengi hawapendi, ndio maana wanapoteza fedha na hawapati maendeleo kwa sababu tabia zao ndio kikwazo cha wao kufanikiwa kifedha.

Kabla sijaendelea na kukuambia mambo ya kufanya ili uwe na tabia ya kuweka akiba na kufanya uwekezaji,tuangalie tabia mbili kubwa za matajiri na watu wenye mafanikio ya kifedha, ambazo ukizijua leo na ukazifanyia kazi utapata matokeo makubwa sana;

  1. Ubahili
    Matajiri wanasifika sana kuwa na tabia ya ubahili sana wa fedha. Hawatoi kabisa fedha zao bila kuwepo na sababu ya msingi kwa sababu wanajua matumizi sahihi ya fedha, kuanzia kuweka bajeti, kupangilia fedha zao, kujilipa kwanza wao wenyewe, wanawekeza fedha zao sehemu ambazo zina faida, kuweka fedha ya dharura na kuishi chini ya kipato!
    Ndio tofauti na maskini ambaye sio bahili, anaendeshwa na hisia, anaishi juu au sawa na kipato chake, hana akiba wala akaunti ya dharura, hana akiba ya kuwekeza, wala hana bajeti binafsi inayoelekeza pesa zake ziende wapi (Pakua app ya Mipangoapp itakusaidia kupanga bajeti ya fedha zako).
    Kua mbahili wa fedha zako!
  2. Hofu
    Hapa nachomaanisha ni kwamba, lazima uwe na lengo la kupata kiwango fulani cha fedha (mafanikio), ambapo ukifikia kiwango hicho, usiingie tamaa ya kutaka fedha zaidi na kupelekea kuhatarisha fedha ambayo umepata ili upate fedha ambayo huna uhakika wa kuipata. Kwani ndio mwanzo wa kupoteza fedha.
    Mfano, umepata faida ya laki moja lakini unataka faida zaidi kwa kuhatarisha fedha ambazo unazo, kwa kuamini utapata kwa kucheza bahati nasibu.
    Unapaswa kuwa na wasiwasi wa kutoruhusu upoteze fedha kirahisi kwa tamaa za faida ya haraka, bali uende kwa mipango na uishi kwa malengo kwenye eneo la fedha. Ndio maana Warren Buffett aliwahi kusema “Ni ujinga wa hali ya juu kupoteza fedha ulizonazo kwa kujiweka kwenye hatari ya kupata fedha nyingi zaidi ambazo huna uhakika wa kupata kwa muda huo” hii yote inasabishwa na kujilinganisha na watu wenye fedha kukuzidi wewe, walizozipata kwa muda mrefu, huku ukitaka kuwa kama wao kwa muda mfupi. Jifunze kulinda fedha zako na kutosheka, kwa wakati huo huku ukijiwekea mkakati endelevu wa kupata fedha zaidi.

Swali Je utajengaje tabia ya kuweka akiba ya fedha zako pamoja na kupata faida ya uwekezaji ambao utafanya?

James Clear kupitia tafiti alieleza kwamba mtu anaweza kujenga tabia yeyote ambayo anataka kwenye maisha yake ndani ya kitabu chake cha “Atomic Habit” ambapo alieleza matabaka matatu ya kujenga tabia (Three layers of behavior change), kupitia matabaka matatu haya utaweza kujenga tabia ya uwekezaji na Kuweka akiba kwenye maisha yako.

Matabaka matatu ya kubadili tabia na kujenga tabia mpya ndani ya siku ishirini na moja (21) na ndani ya siku tisini (90) hadi tabia kuwa sehemu ya maisha yako ni haya;

  1. THE RESULT (MATOKEO)
    Tabaka la kwanza ni matokeo, unajiuliza je ukijenga tabia ya kuwekeza na kuweka akiba utapata faida gani? Namaanisha, kabla ya kuanza kujenga tabia lazima kuwepo na sababu ya kwanini unataka kujenga tabia hiyo. Sababu ya kwanini unataka matokeo ndio yenye kukufanya wewe uwe na hamasa ya kuchukua hatua ili uweze kupata matokeo kupitia sababu ya kwanini. Hivyo, hakikisha unajiuliza kwanini unataka kuelekea uhuru wa kifedha kwa kujenga tabia mpya ya kuweka akiba na kutunza fedha; anza mwisho kuja mwanzo kwa maana matokeo utapata mwisho baada ya kuchukua hatua mwanzoni.

Unataka matokeo yapi kupitia tabia ya kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa faida?

  • Nataka matokeo ili niweze kuelekea uhuru wa kifedha
  • Nataka matokeo ili niwe na maisha mazuri
  • Nataka matokeo ili niweze kuwekeza kwenye biashara.
  • Nataka matokeo ili niweze kuwekeza kwenye ujasiriamali
  • Nataka matokeo ili nisiwe mtu wa madeni
  • Nataka matokeo ili niwekeze kwenye kilimo
  • Nataka matokeo ili niwekeze kwenye huduma na ujuzi nk.

Kwenye hii hatua hakikisha unajiuliza kwanini unataka matokeo kupitia tabia ya kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa faida.

  1. THE PROCESS (MACHAKATO)
    Baada ya kuamua matokeo gani unataka kwenye uwekezaji na Kuweka akiba, ni hatua gani unachukua Ili uweze kupata matokeo ambayo unataka?
    Hapa unaanza kujenga tabia ya Kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa faida kwa kuzingatia mambo yafuatayo kujenga tabia hii;
  • Anza kuongeza maarifa kuhusu elimu ya fedha kila siku.
  • Anza kujilipa mwenyewe kwanza kwenye kila fedha ambayo unapata kabla ya kutumia fedha hizo kwenye matumizi mengine, kwa maana kuweka akiba
  • Anza kuishi chini ya kipato chako, kwa maana matumizi ya fedha zako yawe chini ya kipato chako Ili uweze kujilipa kwanza
  • Anza kuishi kwa bajeti, panga bajeti kwenye maeneo makubwa matano ambayo ni mahitaji ya muhimu, mahitaji yasiyo ya muhimu, kuweka akiba, fungu la kumi na fedha ya dharura
  • Anza kuongeza ufahamu kuhusu uwekezaji kwenye maeneo tofauti tofauti kuanzia hisa, hati fungani, biashara, ujasiriamali, kilimo n.k.

Mwanzoni, kufanya mambo haya itakuwa ngumu sababu haikuwa desturi yako, hivyo lazima uwe na nidhamu ya kutenga akiba na kuwekeza, kila siku ndani ya siku ishirini na moja (21) bila kukosa, ili uzoee kuwa utamaduni.
Huu ndio mwanzo wa kuwa na tabia ya Kuweka AKIBA na kufanya UWEKEZAJI wa faida.

  1. THE IDENTITY (UTAMBULISHO)
    Baada ya kujenga tabia ya Kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa faida, sasa utambulisho wako unabadilika na Kutambulika kama mtu mwenye nidhamu ya fedha na mwekezaji ambaye amewekeza kwenye maeneo mbalimbali.

Hivi ndivyo Mohammed Dewji, Aliko Dangote, Warren Buffett, Jack Ma n.k wanavyotambulika!

Tazama Kanuni hii

AKIBA + UWEKEZAJI = MAFANIKIO.

Ishi na Kanuni kwenye maisha yako ya kila siku kwa kuchukua hatua.

Tunakutakia utekelezaji mwema.

Comments

  • Magreth mangu

    Amazing post

  • John Gastone

    Ahsanteni kwa somo zuri, nimekua nikisoma makala nyingi kuhusu maendeleo ya kifedha ya mtu binafsi( Personal Financial Development) lakini madini niliyoyapata humu ni kuntu. Endeleeni kutupa elimu vijana tuzidi kujenga taifa imara.

  • Mbuya

    Nimepata kitu kikibwa sana Leo

  • Erick Mwibale

    Playback Poa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.