TEL: +255 752 920 592

Ili Ufanikiwe, ni Muhimu kua na mshauri (mentor)!

Wanamichezo wote duniani wanasaidiwa na kocha kujiinua na kua wanamichezo bora na hivyo kufanikiwa katika tasnia yao. Iko hivyo pia kwa wafanyabiashara wenye mafanikio katika biashara na fani zao, ni lazima kua na mtu ambaye ana ujuzi na uzoefu wa unachokifanya wa kukusaidia na kukuongoza ili ufanikiwe!

 

Wengine huwaita watu hawa ‘God Father’. Muhimu ni kutambua umuhimu wa nafasi hii na kutafuta mshauri wako, mmoja hadi watatu na kuwatumia ipasavyo ili kuepuka makosa yasiyo lazima kupitia.

 

Tutapitia njia 10 za jinsi unaweza kumpata mshauri wako na jinsi atakufaa;

 

Tafuta Mtu ambaye ungependa kua kama yeye.

Hii ni hatua ya kwanza na ya muhimu sana, ili umsikilize na kumheshimu mshauri wako, ni muhimu akawa mtu ambaye kibiashara, na kimaisha ungependa kua kama yeye. Ni vyema zaidi akawa na umri wa kukuzidi ili uweze kumtii na anaweza kuwa na ushauri mzuri kwasababu ya uzoefu. Pia itakupa nafasi ya kujiona utakavyokua miaka ya mbele.

Jitahidi mtu huyu awe na maisha unayopenda kua nayo kuanzia aina ya maisha hadi shughuli zake. Kama ungependa kua baba/ mama mwenye familia anayoipenda, kuijali, kuipa kipaombele na mwenye mafanikio makubwa kifedha, basi mshauri wako awe hivyo hivyo.

 

Msome na Umjue Zaidi Mtu Huyo
Hakikisha unamjua mshauri utakayemchagua, vizuri. Uwe na taarifa zake za kutosha. Sisemi umchunguze sana, hapana ila hakikisha unamjua vizuri, kuepuka kukata tamaa baada ya kupata taaarifa zisizokupendeza za kumuhusu baada ya kumsikiliza kwa muda mrefu.
Katika kuchagua mshauri, usitegemee kupata mtu asiye na doa au malaika hapana, kila mtu ana mapungufu yake, ila hakikisha umeyajua na kuyakubali mapungufu ya unayetaka awe mshauri wako.

 

Muombe awe mshauri wako
Baada ya kuridhika na taarifa za uliyechagua kua mshauri wako, hatua inayofuata ni kuonana nae na kumuomba awe mshauri wako.
Unaweza muandikia meseji au kumpigia au kumfuata ana kwa ana kumuomba miadi na wewe siku atakayokua na nafasi au mkutane mahali tulivu ili kuongea vizuri. Epuka kumuomba umshauri kupitia sms/simu au akiwa katika shughuli zake. Onana nae ili muongee akujue na kuamua kama angependa kukusaidia au la. Katika miadi yenu fika kwa wakati, vaa vizuri na jiandae vya kutosha. Maongezi yawe mchanganyiko wa maongezi ya kawaida ‘stori’ na makini ili muelewane na kuzoeana vyema. Ukiona unatumia nguvu nyingi kujenga mazoea au hamjaendana, basi fupisha kikao chenu kuepusha kukwazana.

 

Fanya tathmini ya matokeo unayotegemea
Baada ya kikao chenu, tafakari kama bado ni mtu ambaye ungependa kua kama yeye, kama kuna ya kujifunza zaidi kutoka kwake na kiujumla, kama ni mtu sahihi kupata unayotegemea kujifunza.
Kumbuka ni sawa kabisa kuwa na mshauri mmoja kwa ajili ya masuala ya kibiashara, mshauri mwingine kwa ajili ya masuala ya kifamilia, kiafya nk. Ni ngumu kupata vyote kutoka kwa mtu mmoja. Cha msingi ni kujua nguvu ya mshauri na kujifunza hicho anachokijua Zaidi.

 

Wasiliana nae baada ya kuonana
Baada ya kufanya tathmini yako, wasialiana na mshauri wako kumshukuru kwa kukupa muda wake na kukubali kukusaidia. Kisha panga kikao kinachofuata. Vikao au miadi inayofuata inaweza kua popote ambapo wote mko radhi. Pia sio lazima mazingira yawe rasmi, na mara nyingi jitahidi kumuona maeneo yake ya kazi au ya kumpumzika, kiufupi, mfuate yeye na sio kumtaka yeye akufuate.
Kama baada ya kuonana hujapenda kuendeleza mahusiano na mshauri husika basi mwambie pia, ila tumia lugha nzuri isiyo mfanya ajisikie vibaya. Unaweza kumwambia, “kama hutojali, nimeona muda wako ni mchache sana ukilinganisha na msaada ninaohitaji, hivyo kama hutajali natafuta namna zingine za kujifunza. Ninaomba ridhaa kukuhusisha kimawazo pale nitakapo kwama wakati wowote.”

 

Ruhusu mahusiano yenu yakue taratibu
Sasa umesha konfem mshauri umempata na atakufaa, hatua inyofuata ni kupalilia mahusiano ili aweze kua huru kukushauri an kukusoa wakati wowote na wewe kua huru kumuuliza maswali au kumuhusisha na jambo lako lolote wakati wowote. Mahusiano ya hivi, hujengwa taratibu. Hivyo wekeza muda wako kupaliliana mahusiano hayo. Jitahidi usitumie nguvu sana hadi muhusika kuona kero. Acha yakue bila kutumia nguvu nyingi.

 

Usikasirike anapokupa changamoto
Mshauri kazi yake kubwa ni kukupa changamoto na ushauri, tegemea maongezi ya hivi kua magumu kwa upande wako. Epuka kuonyesha hasira au kuvunjika moyo anapokukosoa au kukupa kazi za ziada, ndio kazi yake. Pokea kukoselewa kwa furaha na kua tayari kubadilika na kusikilza wakati wowote.

 

Fanya Jitihada za kujenga urafiki
Mshauri ni mshkaji wako, rafiki yako hivyo jitahidi kupalilia mazoea ya mahusiano yenu yasiwe rasmi. Muweze kupiga stori, kucheka na kujadiliana mambo binafsi na yasio binafsi. Unatakiwa kufurahia kuonana na mshauri wako na yeye afurahie kuonana na kuzungumza na wewe. Ndio njia pekee ya mahusiano yenu kudumu.

 

Muombe Mrejesho
Jenga tamaduni wa kumuomba mshauri wako mrejesho/ maoni na awe na uhuru wa kukupa mrejesho kama ulivyo. Maoni yatakujenga na kuwezesha kujijua zaidi. Kama ni mshauri wa masuala ya biashara basi kila baada ya miezi mitatu au minne, muulize maoni yake kuhusu wewe kama mfanyabiashara na kama mwanafunzi. Maoni yawe na maelezo ya kutosha na uulize maswali inapobidi ili utoke na funzo la kutosha.
Fanya zoezi hili la maoni hata baada ya kufanikiwa kujifunza uliyotaka kujifunza.

 

Tambua ni mahusiano ya muda mrefu
Mwisho, jua kwamba mahusiano ya mshauri ni ya kudumu, kitakachobadilika ni kupungua kwa aina ya maongezi.

 

Kila la heri katika kutafuta mshauri wako!

Lilian Makoi
Muanzilishi, Mipango Fintech Ltd

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.