TEL: +255 752 920 592

Bidii Bila Kuchoka, Juhudi Zilivyofanikisha Ndoto za Mbwana Samatta Ulaya!

Wengi hususan wapenda michezo, hapana shaka wameshamsikia kijana machachari wa mchezo wa soka, Mbwana Samatta mwenye umri wa miaka 27 tu.
Kijana huyo kutoka Mbagala jijini Dar es Salaam, ni moja ya vielelezo vya watu wachache waliopambana kwa hali na mali kutimiza ndoto zao.
Licha ya kuwa Tanzania imekuwa na wanasoka wengi wenye vipaji, Samatta kwa sasa ndiye kijana wa kuigwa na mfano bora kwenye mafanikio ya soka, hususan baada ya kujiunga na klabu ya Genk ya Ubelgiji na baadaye Aston Villa, inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza, mapema mwaka 2020.
Kwa sasa Samatta, ambaye ni kapteni wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) anachezea timu ya Fenerbahçe S.K.  ya Uturuki kwa mkopo, akitokea Aston Villa.
Pamoja na umaarufu wake, si watu wote wanafahamu safari yake iliyofanikisha kufikia ndoto zake na namna anavyotekeleza mipango yake ya kibiashara.
 
Alianza lini kucheza mpira?
“Nilianzia mtaani. Nikacheza timu za mtaani na nikabahatika kusajiliwa na timu ya Mbagala Market.  Baada ya msimu mmoja klabu ya Simba ilinitaka na baada ya Simba nilipata bahati ya kwenda TP Mazembe,” anasema Samatta.
“Baada ya kutoka TP Mazembe then (baadaye) nilienda Belgium katika timu ya Genk na hatimaye Aston Villa.”
Tofauti na vijana wengi ambao huenda wakabweteka na mafanikio, Samatta anaeleza kuwa safari zake zote za soka siyo safari zinazoweza kumfanya asimame sehemu moja na kuridhika.
“Safari hizi haziwezi kunifanya nisimame sehemu moja na kunifanya nikaridhika kwamba, okay (sawa) kwa mafanikio niliyoyapata nadhani inatosha kwa hiyo naweza nikarelax, no (hapana).”
 
 
Unaweza kuwa unayetaka
“Siku zote naamini kama nimeweza kupanda ngazi moja na naweza kupanda ngazi nyingine pia,” anaeleza.

Mafanikio siku zote hayaji bila changamoto. Je ni masaibu gani amekumbana nayo katika safari yake ya kufikia malengo ya kisoka?

“Changamoto kubwa niliyokutana nayo ni hali ya kuwa Mtanzania kwa sababu kabla yangu hakukuwa na mchezaji wa soka ambaye amepata mafanikio makubwa kiasi cha watu kuweza kukuamini moja kwa moja.
Hata mimi sikuwa naamini kwamba naweza kucheza ligi ya Uingereza. Kwa hiyo juhudi na jitihada nazozionyesha kila wakati, nafikiri zinatengeneza njia kuwafanya watu waamini kuwa kuna Watanzania wengine wanaweza kufanya kitu kama ninachokifanya,” anaeleza Samatta kwa kujiamini na kuongeza;
“Mtu akiniambia ndoto yangu inawezekana moja kwa moja mimi naamini. Kwa sababu mimi leo ninaiishi ndoto yangu.”
 
Panga, ishi ndoto yako
Samatta anasema kuwa katika maisha “kuna vitu vingine ukishindwa kama binadamu ni kawaida lakini ukiwekeza muda wako, ukiongeza juhudi naamini kwamba mwisho wa siku utakuja kujiona umeshinda miaka yote.”
“Nina msemo wangu mmoja napenda sana kuutumia unaitwa “Haina kufeli!”. Haina kufeli ni msemo uliokuja kutokana na kuamini kwamba hakuna kitu ambacho kinachoweza kukuzuia usitimize ndoto yako,” anaeleza.
Kwa Samatta kutoka Mbagala hadi Ulaya ni safari ndefu ambayo kwa mazingira aliyokulia na watu anaocheza nao kwenye ligi hizo za Ulaya, ni tofauti, jambo ambalo huenda lingekatisha tamaa wengi waliokulia Uswahilini.
“Ukiangalia safari nyingi za wachezaji wengi wa Ligi Kuu za Uingereza, wamepitia Academy (shule maalum za michezo) kubwa na mashuhuri. Wamefunzwa na Makocha bora duniani, programu walizopitia zimegharamiwa kwa mamilioni ya dola.
Safari yangu ilikuwa ya tofauti. Nilisaini mkataba wangu kwanza nikiwa na miaka 17 na haikuwa klabu kubwa. Ilikuwa kikosi chetu cha palepale mtaani Mbagala sokoni,” anasema Samatta akielezea kwa undani namna safari yake ilivyoanza ikilinganishwa na wenzie anaocheza nao soka Ulaya.
“Mshahara wangu ulikuwa sifuri. Watanzania huwa wananiuliza najisikiaje kutimiza ndoto zangu na huwa nawaambia kuwa ndoto zangu ndiyo kwanza zinaanza,” anasema.

Samatta anahimiza Zaidi katika kujiwekea malengo na kua na bidi bila kuchoka. Bidii yake ndiyo iliyomfikishe kwenye mafanikio au ulimwengu ambao hakua ameuwaza wakati akijiwekea malengo yake ya mafanikio. “Katika bidii kuna fursa zitajileta kwako, kwani fursa au mafanikio huzunguka duniani zikitafuta mazingira ‘mazuri’ ya kukaa. Mazingira mazuri au yanayo yavutia mafanikio ni mtu mwenye bidii, malengo na nidhamu ya maisha na pesa kwa ujumla. Mafanikio anapozunguka na kuona mazingira kama haya, basi anatia nanga na kukaa hapo kabisa, kwani anajua mazingira haya yatamfanya akae na akue. Tabia za uvivu, kukata tamaa na matumizi hovyo ya pesa, humkimbiza mafanikio kabisa!” alimaliza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

About us

Mipango ni app na tovuti iliyojikita katika kutoa elimu ya kifedha na kuwezesha usimamizi bora wa kifedha, binafsi na kufikia malengo ya kimaendeleo.